Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
2 Samuel 19.13 Bible en Swahili de l’est
1 Kisha Yoabu akaambiwa, Angalia, mfalme anamlilia Absalomu na kumwombolezea. 2 Na kushinda kwao vitani siku ile kukageuzwa kuwa maombolezo kwa watu wote; maana watu walisikia siku ile ya kwamba, Mfalme anahuzunika kwa ajili ya mwanawe. 3 Watu wakajificha siku ile, wakaingia mjini kama vile watu waonao fedheha wajifichavyo, hapo wakimbiapo vitani. 4 Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu! 5 Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako; 6 kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako. 7 Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa Bwana, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hata sasa. 8 Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme. Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake. 9 Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii mbele ya Absalomu.
Retour de David sur le trône
10 Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lo lote juu ya kumrudisha tena mfalme? 11 Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake. 12 Ninyi ni ndugu zangu, ninyi ni mfupa wangu na nyama yangu; mbona basi ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme. 13 Kisha mkamwambie Amasa, Je! Si wewe uliye mfupa wangu, na nyama yangu? Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, usipokuwa wewe jemadari wa jeshi mbele yangu daima mahali pa Yoabu. 14 Akawainamisha mioyo watu wote wa Yuda, kama mtu mmoja; basi wakatuma kwa mfalme, Rudi wewe na watumishi wako wote. 15 Hivyo mfalme akarudi, akafika Yordani. Kisha Yuda wakaja Gilgali kwenda kumlaki mfalme, na kumvusha mfalme Yordani. 16 Akafanya haraka Shimei, mwana wa Gera, Mbenyamini, wa Bahurimu akashuka pamoja na watu wa Yuda ili kumlaki mfalme Daudi. 17 Na Watu elfu wa Benyamini walikuwa pamoja naye, na huyo Siba mtumwa, nyumba ya Sauli, na hao wanawe kumi na watano, na watumwa wake ishirini pamoja naye; wakavuka Yordani mbele ya mfalme. 18 Tena ikavuka mashua ili kuwavusha jamaa ya mfalme, na kufanya aliyoyaona kuwa mema. Ndipo Shimei, mwana wa Gera, akamwangukia mfalme alipokuwa amevuka Yordani. 19 Akamwambia mfalme, Bwana wangu asinihesabie uovu, wala usiyakumbuke yale niliyoyatenda mimi mtumwa wako kwa upotoe siku ile alipotoka Yerusalemu bwana wangu mfalme, hata mfalme ayatie moyoni mwake. 20 Kwa kuwa mimi mtumwa wako najua ya kwamba nimekosa; kwa hiyo, tazama, nimekuja leo, wa kwanza wa nyumba yote ya Yusufu, kushuka ili nimlaki bwana wangu mfalme. 21 Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akajibu na kusema, Je! Shimei hatauawa kwa sababu hii, kwa kuwa amemlaani masihi wa BWANA? 22 Lakini Daudi akasema, Mimi nina nini nanyi, enyi wana wa Seruya, hata mmekuwa adui zangu leo? Je! Atauawa mtu ye yote leo katika Israeli? Kwa maana sijui mimi leo ya kwamba ndimi mfalme juu ya Israeli? 23 Kisha mfalme akamwambia Shimei, Hutakufa. Mfalme akamwapia. 24 Kisha Mefiboshethi, mwana wa Sauli, akashuka ili amlaki mfalme; alikuwa hakukata kucha za miguu yake wala kukata ndevu zake, wala kufua nguo zake, tangu siku alipoondoka mfalme, hata siku hiyo aliporudi kwake kwa amani. 25 Basi ikawa, alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, mfalme akamwambia, Mbona hukwenda pamoja nami, Mefiboshethi? 26 Naye akajibu, Bwana wangu, Ee mfalme, mtumwa wangu alinidanganya; kwa kuwa mimi mtumwa wako nilisema, Nitajitandikia punda, nipate kumpanda, na kwenda pamoja na mfalme; kwa sababu mimi mtumwa wako ni kiwete. 27 Naye amenisingizia mimi mtumwa wako kwa bwana wangu mfalme; lakini bwana wangu mfalme ni kama malaika wa Mungu; utende basi yaliyo mema machoni pako. 28 Kwa kuwa jamaa yote ya baba yangu walikuwa kama watu wa kufa tu mbele ya bwana wangu mfalme; ila uliniweka mimi mtumwa wako kati ya hao walao mezani pako. Basi ni haki gani sasa niliyo nayo, hata nimlilie mfalme zaidi? 29 Basi mfalme akamwambia, Kwa nini unazidi kuyanena mambo yako? Mimi naamua, Wewe na Siba mwigawanye hiyo nchi. 30 Naye Mefiboshethi akamwambia mfalme, Naam, hata yote na atwae yeye, kwa kuwa bwana wangu mfalme amekuja kwa amani nyumbani kwake. 31 Tena Barzilai, Mgileadi, akashuka kutoka Rogelimu; akavuka Yordani pamoja na mfalme, amvushe Yordani. 32 Naye huyo Barzilai alikuwa mzee sana, amepata umri wa miaka themanini; naye amemlisha mfalme hapo alipokuwapo Mahanaimu; kwa kuwa alikuwa mtu mwenye cheo kikubwa. 33 Naye mfalme akamwambia Barzilai, Uvuke pamoja nami; nami nitakulisha kwangu huko Yerusalemu. 34 Lakini Barzilai akamjibu mfalme, Siku ni ngapi za miaka ya maisha yangu, hata mimi nipande pamoja na mfalme kwenda Yerusalemu? 35 Nimepata leo miaka themanini; nami je! Naweza kupambanua mema na mabaya? Mimi mtumwa wako, je! Naweza kuonja nilacho au ninywacho? Naweza kusikia tena sauti ya waimbaji waume na wake? Kwa nini basi mtumwa wako amlemee bado bwana wangu mfalme? 36 Mtumwa wako ataka kuvuka Yordani tu pamoja na mfalme; tena mbona mfalme anilipie thawabu ya namna hii? 37 Niache nirudi basi, mimi mtumwa wako, ili nife katika mji wangu mwenyewe, karibu na kaburi la baba yangu na la mama yangu. Lakini tazama, mtumwa wako Kimhamu; na avuke yeye pamoja na bwana wangu mfalme; nawe ukamtendee yeye yaliyo mema machoni pako. 38 Mfalme akajibu, Haya, Kimhamu na avuke pamoja nami, nami nitamtendea yaliyo mema machoni pako wewe; na kila utakalotaka kwangu, mimi nitalifanya kwa ajili yako. 39 Basi watu wote wakavuka Yordani, naye mfalme akavuka; kisha mfalme akambusu Barzilai, akambariki; naye akarejea mahali pake. 40 Hivyo mfalme akavuka, akafika Gilgali; Kimhamu akavuka pamoja naye; na watu wote wa Yuda wakamvusha mfalme, na nusu ya watu wa Israeli.
Tensions entre Judéens et Israélites
41 Tena, angalia, watu wote wa Israeli wakamjia mfalme wakamwambia mfalme, Kwa nini ndugu zetu, watu wa Yuda wamekuiba, na kumvusha Yordani mfalme, na jamaa yake, na watu wote wa Daudi pamoja naye? 42 Ndipo watu wote wa Yuda wakawajibu hao watu wa Israeli, Ni kwa sababu mfalme ndiye wa jamaa yetu; mbona basi ninyi mmekasirika kwa ajili ya jambo hili? Je! Sisi tumekula kitu cha mfalme? Ama ametupa sisi zawadi yo yote? 43 Hao watu wa Israeli wakawajibu watu wa Yuda, wakasema, Sisi tunazo sehemu kumi katika mfalme, tena tunayo haki yetu katika Daudi zaidi kuliko ninyi; mbona basi ninyi mmetudharau sisi, lisitakwe kwanza shauri letu katika kumrudisha tena mfalme wetu? Na maneno ya watu wa Yuda yakawa makali kuliko maneno ya watu wa Israeli.