Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Deutéronome 1.10 Bible en Swahili de l’est
Rappels et encouragements
Rappel des paroles de l’Éternel à Horeb
1 Haya ndiyo maneno Musa aliyowaambia Israeli wote ng’ambo ya Yordani barani, katika Araba lililoelekea Sufu, kati ya Parani, na Tofeli, na Labani, na Hazerothi, na Dizahabu. 2 Ni mwendo wa siku kumi na moja kutoka Horebu kwa njia ya mlima wa Seiri mpaka Kadesh-barnea. 3 Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na Bwana ya kuwaamuru; 4 alipokwisha kumpiga Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa akikaa Ashtarothi iliyo katika Edrei; 5 ni ng’ambo ya Yordani katika nchi ya Moabu, alipoanza Musa kufunua torati hii, akisema, 6 Bwana, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha; 7 geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati. 8 Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi Bwana aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao. 9 Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu. 10 Bwana, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi. 11 Bwana, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi. 12 Nitachukuaje peke yangu mimi mwenyewe udhia wenu, na mzigo wenu, na mateto yenu? 13 Jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya kabila zenu, nami nitawafanya wawe vichwa juu yenu. 14 Nanyi mkanijibu, mkaniambia, Jambo ulilonena ni jema la kufanya. 15 Basi nikatwaa vichwa vya kabila zenu wenye akili, waliojulikana, nikawafanya wawe vichwa juu yenu, maakida ya elfu elfu, na maakida ya mia mia, na maakida ya hamsini hamsini, na maakida ya kumi kumi, na wenye amri, kwa kadiri ya kabila zenu. 16 Nikawaagiza wakati ule waamuzi wenu, nikawaambia, Sikizeni ninyi maneno kati ya ndugu zenu, mkaamue kwa haki kati ya mtu na nduguye, na mgeni aliye pamoja naye. 17 Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza. 18 Nikawaamuru wakati huo mambo yote yaliyowapasa ninyi kuyafanya.
Incrédulité à Kadès-Barnéa
19 Tukasafiri kutoka Horebu, tukapita katikati ya jangwa lile kubwa la kutisha mliloliona, njia ile ya kuiendea nchi ya vilima vya Waamori, kama Bwana, Mungu wetu, alivyotuamuru, tukafika Kadesh-barnea. 20 Nami nikawaambia, Mmefika nchi ya vilima ya Waamori, anayotupa sisi Bwana, Mungu wetu. 21 Tazama, Bwana, Mungu wako, ameiweka nchi mbele yako; haya panda, itamalaki, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuambia; usiogope wala usifadhaike. 22 Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia. 23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila. 24 Nao wakageuka, wakapanda mlimani wakafika bonde la Eshkoli, wakalipeleleza. 25 Wakatwaa baadhi ya matunda ya nchi ile mikononi mwao, wakatuletea huku chini, wakatuletea habari tena, wakasema, Nchi hii anayotupa Bwana, Mungu wetu, ni nchi njema. 26 Lakini hamkukubali kukwea huko, mlihalifu neno la Bwana, Mungu wenu; 27 mkanung’unika hemani mwenu, mkasema, Ni kwa sababu Bwana ametuchukia, ndipo akatutoa katika nchi ya Misri, apate kututia katika mikono ya Waamori, ili kutuangamiza. 28 Twakwea kwenda wapi? Ndugu zetu wameiyeyusha mioyo yetu, wakituambia, Wale watu ni wengi, ni warefu kuliko sisi; miji nayo ni mikubwa, imejengewa kuta hata mbinguni; na zaidi ya hayo huko tumewaona Waanaki. 29 Ndipo nikawaambieni, Msifanye hofu, wala msiwache. 30 Bwana, Mungu wenu, anayetangulia mbele yenu, ndiye atakayewapigania, kwa mfano wa yote aliyowafanyia huko Misri mbele ya macho yenu; 31 na huko jangwani, ulipoona alivyokuchukua Bwana, Mungu wako, kama mtu amchukuavyo mwanawe, njia yote mliyoiendea, hata mkafikilia mahali hapa. 32 Lakini katika jambo hili hamkumwamini Bwana, Mungu wenu, 33 aliyewatangulia njiani, usiku kwa moto, kuwaonyesha njia mtakayoiendea, na mchana kwa hilo wingu, ili apate kuwatafutia mahali pa kusimamisha hema zenu. 34 Bwana akaisikia sauti ya maneno yenu, akaghadhibika, akaapa, akasema, 35 Hakika yangu hapana mmoja miongoni mwa watu hawa wa kizazi hiki kibaya atakayeiona nchi hiyo nzuri, niliyowaapia baba zenu kuwapa, 36 isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, huyo ataiona; nami nitampa yeye na watoto wake nchi hiyo aliyoikanyaga; kwa kuwa amemfuata Bwana kwa kila neno. 37 Na Bwana alinikasirikia mimi kwa ajili yenu, akasema, Wala wewe hutaingia humo; 38 Yoshua mwana wa Nuni asimamaye mbele yako ndiye atakayeingia; mtie moyo; kwa kuwa yeye atawarithisha Israeli. 39 Tena, wadogo wenu, mliosema watakuwa mateka, na wana wenu, wasiokuwa leo na maarifa ya mabaya wala mema, ndio watakaoingia, nao ndio nitakaowapa, nao wataimiliki. 40 Na ninyi basi geukeni, mshike safari yenu, mwende jangwani kwa njia ya Bahari ya Shamu. 41 Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya Bwana, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na Bwana. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. 42 Bwana akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. 43 Basi niliwaambia, msinisikize, bali mliasi amri ya Bwana, mkajikinai, na kukwea mlimani. 44 Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma. 45 Mkarudi mkalia mbele za Bwana; Bwana asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu. 46 Ndipo mkakaa Kadeshi siku nyingi, kwa kadiri ya hizo siku mlizokaa.