Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Jean 16.11 Bible en Swahili de l’est
Voir Jean 16.1 en vidéo
1 Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. 2 Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. 3 Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. 4 Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia. Sikuwaambia hayo tangu mwanzo, kwa sababu nalikuwapo pamoja nanyi. 5 Lakini sasa mimi naenda zangu kwake yeye aliyenipeleka, wala hakuna mmoja wenu aniulizaye, Unakwendapi? 6 Ila kwa sababu nimewaambia hayo huzuni imejaa mioyoni mwenu. 7 Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. 8 Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. 9 Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; 10 kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; 11 kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa. 12 Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa. 13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. 14 Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. 15 Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.
Voir Jean 16.16 en vidéo
16 Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni; na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona. 17 Basi baadhi ya wanafunzi wake wakasemezana, Neno gani hilo asemalo, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? Na hilo, Kwa sababu naenda zangu kwa Baba? 18 Basi walisema, Neno gani hilo asemalo; hilo, Bado kitambo kidogo? Hatujui asemalo. 19 Yesu alifahamu ya kwamba wanataka kumwuliza, akawaambia, Ndilo hilo mnaloulizana, ya kuwa nalisema, Bado kitambo kidogo nanyi hamnioni, na tena bado kitambo kidogo nanyi mtaniona? 20 Amin, amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha. 21 Mwanamke azaapo, yuna huzuni kwa kuwa saa yake imefika; lakini akiisha kuzaa mwana, haikumbuki tena ile dhiki, kwa sababu ya furaha ya kuzaliwa mtu ulimwenguni. 22 Basi ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye. 23 Tena siku ile hamtaniuliza neno lo lote. Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu. 24 Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu. 25 Hayo nimesema nanyi kwa mithali; saa yaja ambapo sitasema nanyi tena kwa mithali, lakini nitawapa waziwazi habari ya Baba. 26 Na siku ile mtaomba kwa jina langu, wala siwaambii ya kwamba mimi nitawaombea kwa Baba; 27 kwa maana Baba mwenyewe awapenda kwa kuwa ninyi mmenipenda mimi, na kusadiki ya kwamba mimi nalitoka kwa Baba. 28 Nalitoka kwa Baba, nami nimekuja hapa ulimwenguni; tena nauacha ulimwengu; na kwenda kwa Baba. 29 Basi wanafunzi wake wakasema, Tazama, sasa wasema waziwazi, wala huneni mithali yo yote. 30 Sasa tumejua ya kuwa wewe wafahamu mambo yote, wala huna haja ya mtu akuulize; kwa hiyo twasadiki ya kwamba ulitoka kwa Mungu. 31 Yesu akawajibu, Je! Mnasadiki sasa? 32 Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa kuwa Baba yupo pamoja nami. 33 Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.