Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

2 Rois 4.10
Bible en Swahili de l’est


1 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa. 2 Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta. 3 Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. 4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. 5 Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina. 6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma. 7 Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako. 8 Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula. 9 Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu. 10 Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo. 11 Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala. 12 Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake. 13 Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe. 14 Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. 15 Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. 16 Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. 17 Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia. 18 Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao. 19 Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake. 20 Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa. 21 Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka. 22 Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena. 23 Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno. 24 Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia. 25 Basi akaenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu, katika mlima wa Karmeli. Ikawa, yule mtu wa Mungu alipomwona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, Tazama, Mshunami yule kule. 26 Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo. 27 Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na Bwana amenificha, wala hakuniambia. 28 Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye? 29 Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto. 30 Na mama yake yule mtoto akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata. 31 Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka. 32 Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake. 33 Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba Bwana. 34 Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake, na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake; mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto. 35 Kisha akarudi, akatembea nyumbani, huko na huko mara moja; akapanda, akajinyosha juu yake; na yule mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake. 36 Akamwita Gehazi, akasema, Mwite yule Mshunami. Basi akamwita. Na alipofika kwake, Elisha akasema, Haya! Mchukue mwanao. 37 Ndipo akaingia, akamwangukia miguu akainama mpaka nchi; kisha akamchukua mwanawe, akatoka. 38 Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii. 39 Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua. 40 Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula. 41 Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani. 42 Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale. 43 Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza. 44 Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

Cette Bible est dans le domaine public.