Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 33.30 Bible en Swahili de l’est
1 Walakini, Ayubu, nakuomba usikilize matamko yangu, Ukayasikilize maneno yangu yote. 2 Tazama basi, nimefunua kinywa changu, Ulimi wangu umenena kinywani mwangu. 3 Maneno yangu yatatamka uelekevu wa moyo wangu; Na hayo niyajuayo midomo yangu itayanena kwa unyofu. 4 Roho ya Mungu imeniumba, Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai. 5 Kwamba waweza, nijibu; Yapange maneno yako sawasawa mbele yangu, usimame. 6 Tazama, mimi ni mbele ya Mungu kama ulivyo wewe; Mimi nami nilifinyangwa katika udongo. 7 Tazama, utisho wangu hautakutia hofu wewe, Wala sitakulemea kwa uzito. 8 Hakika umenena masikioni mwangu, Nami nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema, 9 Mimi ni safi, sina makosa; Sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu; 10 Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami, Hunihesabu kuwa ni adui yake; 11 Hunitia miguu yangu katika mkatale, Na mapito yangu yote huyapeleleza. 12 Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki; Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu. 13 Nawe kwani kumnung’unikia, Kwa vile asivyotoa hesabu ya mambo yake yote? 14 Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. 15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; 16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, 17 Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; 18 Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga. 19 Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake; 20 Hata roho yake huchukia chakula, Na nafsi yake huchukia nyama nzuri. 21 Nyama ya mwili wake huliwa, isionekane; Na mifupa yake isiyoonekana yatokea nje. 22 Naam, nafsi yake inakaribia shimoni, Na uhai wake unakaribia waangamizi. 23 Kwamba akiwapo malaika pamoja naye, Mkalimani, mmoja katika elfu, Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo; 24 Ndipo amwoneapo rehema, na kusema, Mwokoe asishuke shimoni; Mimi nimeuona ukombozi. 25 Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto; Huzirudia siku za ujana wake; 26 Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia; Hata auone uso wake kwa furaha; Naye humrejezea mtu haki yake. 27 Yeye huimba mbele ya watu, na kusema, Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea, Wala sikulipizwa jambo hilo; 28 Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni, Na uhai wangu utautazama mwanga. 29 Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya, Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu,30 Ili kurudisha roho yake itoke shimoni, Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai.31 Angalia sana, Ee Ayubu, unisikilize; Nyamaza, mimi nitasema. 32 Kama una neno la kusema, nijibu; Nena, kwani nataka kukuhesabia kuwa na haki. 33 Kama sivyo, unisikilize mimi; Nyamaza, nami nitakufunza hekima.