Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Ezéchiel 18.12 Bible en Swahili de l’est
On récolte ce qu’on sème
1 Neno la Bwana likanijia tena, kusema, 2 Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno? 3 Kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hamtakuwa na sababu ya kuitumia tena mithali hii katika Israeli. 4 Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa. 5 Bali kama mtu ni mwenye haki, na kuyatenda yaliyo halali na haki; 6 hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, wala hakumkaribia mwanamke wakati wa kutengwa kwake; 7 wala hakumdhulumu mtu, bali amemrudishia mdeni wake rehani yake, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, naye amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwavika nguo walio uchi; 8 ambaye hakumkopesha mtu ili apate faida, wala hakupokea ziada ya namna yo yote; naye ameuepusha mkono wake na uovu, na kufanya hukumu ya haki kati ya mtu na mwenzake; 9 tena ikiwa amezifuata sheria zangu, na kuzishika hukumu zangu; mtu huyu ni mwenye haki; hakika ataishi, asema Bwana MUNGU. 10 Walakini akizaa mwana aliye mnyang’anyi, mmwaga damu, atendaye mambo hayo mojawapo; 11 wala hakutenda mojawapo la mambo hayo yampasayo, bali amekula juu ya milima, na kumtia unajisi mke wa jirani yake, 12 na kuwadhulumu maskini na wahitaji, na kuwanyang’anya watu mali yao kwa nguvu, wala hakurudisha rehani, naye ameviinulia macho vinyago, na kufanya machukizo, 13 naye amekopesha watu ili apate faida, na kupokea ziada; je! Ataishi baada ya hayo? La, hataishi; amefanya machukizo hayo yote; hakika atakufa; damu yake itakuwa juu yake. 14 Na kama yeye huyo akizaa mwana, naye ameona dhambi zote za baba yake alizozitenda, akaogopa, asifanye neno lo lote kama hayo; 15 hakula juu ya milima, wala hakuviinulia macho vinyago vya nyumba ya Israeli, wala hakumtia unajisi mke wa jirani yake, 16 wala hakumdhulumu mtu, wala hakutwaa kitu kiwekwe rehani, wala hakumnyang’anya mtu mali yake kwa nguvu, bali amewapa wenye njaa chakula chake, na kuwafunika nguo walio uchi; 17 tena ikiwa ameuzuia mkono wake asimwonee maskini, wala hakupokea faida na ziada, naye amezifanya hukumu zangu, na kuzifuata sheria zangu; hatakufa huyu kwa sababu ya uovu wa baba yake, hakika ataishi. 18 Kwa habari za yule baba yake, kwa sababu aliwaonea watu kwa ukali mwingi, na kumnyang’anya ndugu yake mali yake kwa nguvu; na kuyatenda yasiyo mema kati ya watu wake, tazama, atakufa katika uovu wake. 19 Lakini ninyi mwasema, Kwani yule mwana asiuchukue uovu wa baba yake? Yule mwana atakapofanya yaliyo halali na haki, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, hakika ataishi. 20 Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake. 21 Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. 22 Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. 23 Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana MUNGU; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi? 24 Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, naam, katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. 25 Lakini ninyi mwasema, Njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, Enyi nyumba ya Israeli; Je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? 26 Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, akafa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. 27 Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. 28 Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa. 29 Lakini nyumba ya Israeli husema, Njia ya Bwana si sawa. Ee nyumba ya Israeli, je! Njia zangu sizo zilizo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? 30 Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. 31 Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, enyi nyumba ya Israeli? 32 Maana mimi sikufurahii kufa kwake afaye, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.