Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Marc 3.28
Bible en Swahili de l’est


1 Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;
2 wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.
3 Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.
4 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.
5 Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena.
6 Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza.
7 Naye Yesu akajitenga, yeye na wanafunzi wake, akaenda baharini. Mkutano mkuu ukamfuata, kutoka Galilaya, na Uyahudi,
8 na Yerusalemu, na Idumaya, na ng’ambo ya Yordani, na pande za Tiro na Sidoni, mkutano mkuu, waliposikia habari za mambo yote aliyokuwa akiyatenda, wakamwendea.
9 Akawaambia wanafunzi wake ya kwamba chombo kidogo kikae karibu naye, kwa sababu ya mkutano, wasije wakamsonga.
10 Maana aliponya wengi, hata wote waliokuwa na misiba wakamrukia wapate kumgusa.
11 Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu.
12 Akawakataza sana, wasimdhihirishe.

Choix des douze apôtres

13 Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea.
14 Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri,
15 tena wawe na amri ya kutoa pepo.
16 Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina la Petro;
17 na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohana nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo;
18 na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Thadayo, na Simoni Mkananayo,
19 na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti. Kisha akaingia nyumbani.

Jésus contesté

20 Mkutano wakakusanyika tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate.
21 Jamaa zake walipopata habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili.
22 Nao waandishi walioshuka kutoka Yerusalemu wakasema, Ana Beelzebuli, na, Kwa mkuu wa pepo huwatoa pepo.
23 Akawaita, akawaambia kwa mifano, Awezaje Shetani kumtoa Shetani?
24 Na ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, ufalme huo hauwezi kusimama;
25 na nyumba ikifitinika juu ya nafsi yake, nyumba hiyo haiwezi kusimama.
26 Na kama Shetani ameondoka juu ya nafsi yake, akafitinika, hawezi kusimama, bali huwa na kikomo.
27 Hawezi mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu, na kuviteka vitu vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu; ndipo atakapoiteka nyumba yake.
28 Amin, nawaambia, Dhambi zote watasamehewa wanadamu, na kufuru zao watakazokufuru zote;
29 bali mtu atakayemkufuru Roho Mtakatifu hana msamaha hata milele; ila atakuwa ana dhambi ya milele,
30 kwa vile walivyosema, Ana pepo mchafu.
31 Wakaja mamaye na nduguze; wakasimama nje, wakatuma mtu kumwita.
32 Na makutano walikuwa wameketi, wakimzunguka, wakamwambia, Tazama, mama yako na ndugu zako wako nje, wanakutafuta.
33 Akawajibu, akisema, Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani?
34 Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!
35 Kwa maana mtu ye yote atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama yangu.

Cette Bible est dans le domaine public.