Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Psaumes 18.13
Bible en Swahili de l’est


1 Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana; 2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu. 3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu. 4 Kamba za mauti zilinizunguka, Mafuriko ya uovu yakanitia hofu. 5 Kamba za kuzimu zilinizunguka, Mitego ya mauti ikanikabili. 6 Katika shida yangu nalimwita Bwana, Na kumlalamikia Mungu wangu. Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake, Kilio changu kikaingia masikioni mwake. 7 Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka, Misingi ya milima ikasuka-suka; Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu. 8 Kukapanda moshi kutoka puani mwake, Moto ukatoka kinywani mwake ukala, Makaa yakawashwa nao. 9 Aliziinamisha mbingu akashuka, Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake. 10 Akapanda juu ya kerubi akaruka, Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo. 11 Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha, Kuwa hema yake ya kumzunguka. Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni. 12 Toka mwangaza uliokuwa mbele zake Kukapita mawingu yake makuu. Mvua ya mawe na makaa ya moto. 13 Bwana alipiga radi mbinguni, Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake, Mvua ya mawe na makaa ya moto. 14 Akaipiga mishale yake akawatawanya, Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya. 15 Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji, Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa, Ee Bwana, kwa kukemea kwako, Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako. 16 Alipeleka kutoka juu akanishika, Na kunitoa katika maji mengi. 17 Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi. 18 Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini Bwana alikuwa tegemeo langu. 19 Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. 20 Bwana alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. 21 Maana nimezishika njia za Bwana, Wala sikumwasi Mungu wangu. 22 Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu, Wala amri zake sikujiepusha nazo. 23 Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake, Nikajilinda na uovu wangu. 24 Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake. 25 Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; 26 Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. 27 Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa, Na macho ya kiburi utayadhili. 28 Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu; Bwana Mungu wangu aniangazia giza langu. 29 Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi, Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta. 30 Mungu, njia yake ni kamilifu, Ahadi ya Bwana imehakikishwa, Yeye ndiye ngao yao. Wote wanaomkimbilia. 31 Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu? 32 Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu, Naye anaifanya kamilifu njia yangu. 33 Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu, Na kunisimamisha mahali pangu pa juu. 34 Ananifundisha mikono yangu vita, Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba. 35 Nawe umenipa ngao ya wokovu wako, Mkono wako wa kuume umenitegemeza, Na unyenyekevu wako umenikuza. 36 Umezifanyizia nafasi hatua zangu, Na miguu yangu haikuteleza. 37 Nitawafuatia adui zangu na kuwapata, Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe. 38 Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu. 39 Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita, Hunitiishia chini yangu walioniondokea. 40 Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo, Nao walionichukia nimewakatilia mbali. 41 Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa, Walimwita Bwana lakini hakuwajibu, 42 Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo, Nikawatupa nje kama matope ya njiani. 43 Umeniokoa na mashindano ya watu, Umenifanya niwe kichwa cha mataifa. Watu nisiowajua walinitumikia. 44 Kwa kusikia tu habari zangu, Mara wakanitii. Wageni walinijia wakinyenyekea. 45 Wageni nao walitepetea, Walitoka katika ngome zao wakitetemeka. 46 Bwana ndiye aliye hai; Na ahimidiwe mwamba wangu; Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu; 47 Ndiye Mungu anipatiaye kisasi; Na kuwatiisha watu chini yangu. 48 Huniponya na adui zangu; Naam, waniinua juu yao walioniinukia, Na kuniponya na mtu wa jeuri. 49 Basi, Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa, Nami nitaliimbia jina lako. 50 Ampa mfalme wake wokovu mkuu, Amfanyia fadhili masihi wake,Daudi na mzao wake hata milele.

Cette Bible est dans le domaine public.