Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Matthieu 24.10 Bible en Swahili de l’est
Discours sur le mont des Oliviers
Destruction de Jérusalem et retour du Fils de l’homme
Voir Matthieu 24.1 en vidéo
1 Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. 2 Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. 3 Hata alipokuwa ameketi katika mlima wa Mizeituni, wanafunzi wake wakamwendea kwa faragha, wakisema, Tuambie, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini dalili ya kuja kwako, na ya mwisho wa dunia? 4 Yesu akajibu, akawaambia, Angalieni, mtu asiwadanganye. 5 Kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ni Kristo; nao watadanganya wengi. 6 Nanyi mtasikia habari za vita na matetesi ya vita; angalieni, msitishwe; maana hayo hayana budi kutukia; lakini ule mwisho bado. 7 Kwa maana taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na njaa, na matetemeko ya nchi mahali mahali. 8 Hayo yote ndiyo mwanzo wa utungu. 9 Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. 10 Ndipo wengi watakapojikwaa, nao watasalitiana, na kuchukiana. 11 Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. 12 Na kwa sababu ya kuongezeka maasi, upendo wa wengi utapoa. 13 Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. 14 Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. 15 Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), 16 ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani; 17 naye aliye juu ya dari asishuke kuvichukua vitu vilivyomo nyumbani mwake; 18 wala aliye shambani asirudi nyuma kuichukua nguo yake. 19 Ole wao wenye mimba na wanyonyeshao siku hizo! 20 Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato. 21 Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. 22 Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo. 23 Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki. 24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule. 25 Tazama, nimekwisha kuwaonya mbele. 26 Basi wakiwaambia, Yuko jangwani, msitoke; yumo nyumbani, msisadiki. 27 Kwa maana kama vile umeme utokavyo mashariki ukaonekana hata magharibi, hivyo ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 28 Kwa kuwa po pote ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai. 29 Lakini mara, baada ya dhiki ya siku zile, jua litatiwa giza, na mwezi hautatoa mwanga wake, na nyota zitaanguka mbinguni, na nguvu za mbinguni zitatikisika; 30 ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni; ndipo mataifa yote ya ulimwengu watakapoomboleza, nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi. 31 Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.
Voir Matthieu 24.32 en vidéo
32 Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu; 33 nanyi kadhalika, myaonapo hayo yote, tambueni ya kuwa yu karibu, milangoni. 34 Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia. 35 Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Appel à la vigilance
36 Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake. 37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 38 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, 39 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. 40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; 41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. 42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. 43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. 44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. 45 Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? 46 Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo. 47 Amin, nawaambieni, atamweka juu ya vitu vyake vyote. 48 Lakini mtumwa yule mbaya akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia; 49 akaanza kuwapiga wajoli wake, na kula na kunywa pamoja na walevi; 50 bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani, na saa asiyojua, 51 atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wanafiki; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.