Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Job 38.32 Bible en Swahili de l’est
1 Ndipo Bwana akamjibu Ayubu katika upepo wa kisulisuli, na kusema, 2 Ni nani huyu atiaye mashauri giza Kwa maneno yasiyo na maarifa? 3 Basi jifunge viuno kama mwanamume, Maana nitakuuliza neno, nawe niambie. 4 Ulikuwa wapi nilipoiweka misingi ya nchi? Haya! Sema, kama ukiwa na ufahamu. 5 Ni nani aliyeamrisha vipimo vyake, kama ukijua? Au ni nani aliyenyosha kamba juu yake? 6 Misingi yake ilikazwa juu ya kitu gani? Au ni nani aliyeliweka jiwe lake la pembeni, 7 Hapo nyota za asubuhi zilipoimba pamoja, Na wana wote wa Mungu walipopiga kelele kwa furaha? 8 Au ni nani aliyeifunga bahari kwa milango, Hapo ilipofurika kana kwamba imetoka tumboni. 9 Nilipolifanya wingu kuwa vazi lake, Na giza zito kuwa nguo ya kuifungia, 10 Nikaiagiza amri yangu; Nikaiwekea makomeo na milango, 11 Nikasema, Utafika mpaka hapa, lakini hutapita, Na hapa mawimbi yako yanyetayo yatazuiliwa? 12 Je! Umeiamuru asubuhi tangu siku zako zilipoanza? Umeyajulisha mapambazuko mahali pake? 13 Yapate kuishika miisho ya nchi, Waovu wakung’utwe wakawe mbali nayo? 14 Hubadilika mfano wa udongo chini ya muhuri, Vitu vyote vinatokea kama mavazi. 15 Na waovu nuru yao huzuiliwa isiwafikie, Na mkono ulioinuka huvunjika. 16 Je! Umeziingia chemchemi za bahari, Au umetembea mahali pa siri pa vilindi? 17 Je! Umefunuliwa malango ya mauti, Au umeyaona malango ya kuzimu? 18 Umeyafahamu mapana ya dunia? Haya! Sema, ikiwa unayajua hayo yote. 19 Iko wapi njia ya kuyafikia makao ya nuru? Na giza pia, mahali pake ni wapi? 20 Upate kuipeleka hata mpaka wake, Upate kuelewa na mapito ya kuiendea nyumba yake? 21 Hukosi unajua, maana ulizaliwa wakati huo, Na hesabu ya siku zako ni kubwa! 22 Je! Umeziingia ghala za theluji, Au umeziona ghala za mvua ya mawe, 23 Nilizoziweka akiba kwa wakati wa misiba, Kwa siku ya mapigano na vita? 24 Je! Nuru hutengwa kwa njia gani, Au upepo wa mashariki hutawanywaje juu ya nchi? 25 Ni nani aliyepasua mfereji kwa maji ya gharika, Au njia kwa umeme wa radi; 26 Kunyesha mvua juu ya nchi isiyo na watu; Juu ya jangwa asiyokaa mwanadamu; 27 Kuishibisha nchi iliyo kame na ukiwa, Na kuyameza majani yaliyo mororo? 28 Je! Mvua ina baba? Au ni nani aliyeyazaa matone ya umande? 29 Barafu ilitoka katika tumbo la nani? Na sakitu ya mbinguni ni nani aliyeizaa? 30 Maji hugandamana kama jiwe, Na uso wa vilindi huganda kwa baridi. 31 Je! Waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia, Au kuvilegeza vifungo vya Orioni?32 Je! Waweza kuziongoza Sayari kwa wakati wake? Au waweza kuongoza Dubu na watoto wake?33 Je! Unazijua amri zilizoamuriwa mbingu? Waweza kuyathibitisha mamlaka yake juu ya dunia? 34 Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni, ili wingi wa maji ukufunikize? 35 Waweza kuutuma umeme, nao ukaenda, Ukakuambia, Sisi tupo hapa? 36 Je! Ni nani aliyetia hekima moyoni? Au ni nani aliyetia ufahamu rohoni? 37 Ni nani awezaye kuyahesabu mawingu kwa hekima? Au ni nani awezaye kuzimimina chupa za mbinguni? 38 Wakati mavumbi yagandamanapo, Na madongoa kushikamana pamoja? 39 Je! Utamwindia simba mke mawindo? Au utashibisha njaa ya simba wachanga, 40 Waoteapo mapangoni mwao, Wakaapo mafichoni wapate kuvizia? 41 Ni nani anayempatia kunguru chakula, Makinda yake wanapomlilia Mungu, Na kutanga-tanga kwa kutindikiwa na chakula?