Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Marc 10.12 Bible en Swahili de l’est
1 Akaondoka huko akafika mipakani mwa Uyahudi, na ng’ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. 2 Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. 3 Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? 4 Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. 5 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. 6 Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. 7 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; 8 na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. 9 Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. 10 Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. 11 Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake;12 na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.13 Basi wakamletea watoto wadogo ili awaguse; wanafunzi wake wakawakemea. 14 Ila Yesu alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa Mungu ni wao. 15 Amin, nawaambieni, Ye yote asiyeukubali ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo hatauingia kabisa. 16 Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia. 17 Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? 18 Yesu akamwambia, Kwa nini kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. 19 Wazijua amri, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama yako. 20 Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. 21 Yesu akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda, ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. 22 Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. 23 Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! 24 Wanafunzi wakashangaa kwa maneno yake. Yesu akajibu tena, akawaambia, Watoto, jinsi ilivyo shida wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa Mungu! 25 Ni rahisi ngamia kupenya katika tundu ya sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. 26 Nao wakashangaa mno, wakimwambia, Ni nani, basi, awezaye kuokoka? 27 Yesu akawakazia macho, akasema, Kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yawezekana kwa Mungu. 28 Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe. 29 Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, 30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele. 31 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho; na wa mwisho watakuwa wa kwanza. 32 Nao walikuwako njiani, huku wakipanda kwenda Yerusalemu; na Yesu alikuwa akiwatangulia, wakashangaa, nao katika kufuata wakaogopa. Akawatwaa tena wale Thenashara, akaanza kuwaambia habari za mambo yatakayompata, 33 akisema, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi, nao watamhukumu afe, watamtia mikononi mwa Mataifa, 34 nao watamdhihaki, na kumtemea mate, na kumpiga mijeledi, na kumwua; na baada ya siku tatu atafufuka. 35 Na Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, wakamwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lo lote tutakalokuomba. 36 Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? 37 Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. 38 Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? 39 Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; 40 lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. 41 Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. 42 Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. 43 Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, 44 na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. 45 Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi. 46 Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia. 47 Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu. 48 Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu. 49 Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita. 50 Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu. 51 Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. 52 Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.