Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Luc 8.51 Bible en Swahili de l’est
Voir Luc 8.1 en vidéo
1 Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye, 2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba, 3 na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.
Le semeur et les terrains
4 Mkutano mkuu ulipokutanika, na wale waliotoka kila mji wakimjia, alisema kwa mfano; 5 Mpanzi alitoka kwenda kupanda mbegu zake; naye alipokuwa akizipanda, nyingine zilianguka karibu na njia, zikakanyagwa, ndege wa angani wakazila. 6 Nyingine zikaanguka penye mwamba; zilipoanza kumea zikakauka kwa kukosa rutuba. 7 Nyingine zikaanguka kati ya miiba, na miiba ikamea pamoja nazo ikazisonga. 8 Nyingine zikaanguka penye udongo mzuri; zikamea, zikazaa moja kwa mia. Alipokuwa akinena hayo alipaza sauti akisema, Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie. 9 Wanafunzi wake wakamwuliza, Maana yake nini mfano huo? 10 Akasema, Ninyi mmepewa kuzijua siri za ufalme wa Mungu; bali wengine kwa mifano, ili wakiona wasione, na wakisikia wasielewe. 11 Na huo mfano, maana yake ni hii; Mbegu ni neno la Mungu. 12 Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka. 13 Na wale penye mwamba ndio wale ambao wasikiapo hulipokea lile neno kwa furaha; nao hawana mizizi, huamini kitambo kidogo, na wakati wa kujaribiwa hujitenga. 14 Na zilizoanguka penye miiba ni wale waliosikia, na katika kuenenda kwao husongwa na shughuli na mali, na anasa za maisha haya, wasiivishe lo lote. 15 Na zile penye udongo mzuri, ndio wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao hulisikia neno, na kulishika; kisha huzaa matunda kwa kuvumilia. 16 Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka mvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. 17 Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. 18 Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho. 19 Wakamwendea mama yake na ndugu zake, wasiweze kumkaribia kwa sababu ya mkutano. 20 Akaletewa habari akiambiwa, Mama yako na ndugu zako wamesimama nje wakitaka kuonana nawe. 21 Akawajibu akasema, Mama yangu na ndugu zangu ndio hao walisikiao neno la Mungu na kulifanya.
Jésus, plus fort que la nature et les démons
Voir Luc 8.22 en vidéo
22 Ikawa siku zile mojawapo alipanda chomboni yeye na wanafunzi wake, akawaambia, Na tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa. Wakatweka matanga. 23 Nao walipokuwa wakienda, alilala usingizi. Ikashuka tufani juu ya ziwa, chombo kikaanza kujaa maji, wakawa katika hatari. 24 Wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana mkubwa, Bwana mkubwa, tunaangamia. Akaamka, akaukemea upepo na msukosuko wa maji, vikakoma; kukawa shwari. 25 Akawaambia, Imani yenu iko wapi? Wakaogopa, wakamaka, wakisema wao kwa wao, Ni nani huyu basi hata anaamuru upepo na maji, navyo vyamtii? 26 Wakafika pwani ya nchi ya Wagerasi, inayoelekea Galilaya. 27 Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. 28 Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. 29 Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. 30 Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. 31 Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. 32 Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. 33 Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. 34 Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. 35 Watu wakatoka kwenda kuliona lililotokea, wakamwendea Yesu, wakamwona mtu yule aliyetokwa na pepo ameketi miguuni pa Yesu, amevaa nguo, ana akili zake; wakaogopa. 36 Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza jinsi alivyoponywa yule aliyepagawa na pepo. 37 Na jamii ya watu wa nchi ya Wagerasi iliyo kando kando walimwomba aondoke kwao, kwa kuwa walishikwa na hofu nyingi; basi akapanda chomboni, akarudi. 38 Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, 39 Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu.
Guérison d’une femme et résurrection d’une fillette
Voir Luc 8.40 en vidéo
40 Basi Yesu aliporudi mkutano ulimkaribisha kwa furaha, maana walikuwa wakimngojea wote. 41 Na tazama, mtu mmoja akaja, jina lake Yairo, naye ni mtu mkuu wa sinagogi, akaanguka miguuni pa Yesu, akamsihi aingie nyumbani kwake; 42 kwa kuwa binti yake yu katika kufa, ambaye ni mwana pekee, umri wake amepata miaka kumi na miwili. Na alipokuwa akienda makutano walimsonga. 43 Na mwanamke mmoja, ambaye ametokwa na damu muda wa miaka kumi na miwili, [aliyekuwa amegharimiwa mali zake zote kwa kuwapa waganga] asipate kuponywa na mtu ye yote, 44 alikwenda nyuma yake, akaugusa upindo wa vazi lake; na mara hiyo kutoka damu kwake kulikoma. 45 Yesu akasema, Ni nani aliyenigusa? Basi, watu wote walipokana, Petro alimwambia, Bwana mkubwa, makutano haya wanakuzunguka na kukusonga. 46 Yesu akasema, Mtu alinigusa, maana naona ya kuwa nguvu zimenitoka. 47 Yule mwanamke, alipoona ya kwamba hawezi kusitirika akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa, na jinsi alivyoponywa mara. 48 Akamwambia Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani. 49 Alipokuwa akinena hayo, alikuja mtu kutoka nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akamwambia, Binti yako amekwisha kufa; usimsumbue mwalimu. 50 Lakini Yesu aliposikia hayo, alimjibu, Usiwe na hofu, amini tu, naye ataponywa. 51 Alipofika nyumbani hakuacha mtu kuingia pamoja naye ila Petro, na Yohana, na Yakobo, na babaye yule mtoto na mamaye. 52 Na watu wote walikuwa wakilia na kumwombolezea; akasema, Msilie, hakufa huyu, bali amelala usingizi tu. 53 Wakamcheka sana, maana walijua ya kuwa amekwisha kufa. 54 Akamshika mkono, akapaza sauti, akisema Kijana, inuka. 55 Roho yake ikamrejea, naye mara hiyo akasimama. Akaamuru apewe chakula. 56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini akawakataza wasimwambie mtu lililotukia.