Fermer le panneau de recherche

Appuyez sur Entrée pour rechercher ou ESC pour annuler.

Luc 9.41
Bible en Swahili de l’est


1 Akawaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. 2 Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. 3 Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. 4 Na nyumba yo yote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke mjini. 5 Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo, yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. 6 Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri injili, na kupoza watu kila mahali. 7 Na Herode mfalme akasikia habari za yote yaliyotendeka, akafadhaika kwa sababu watu wengine walisema ya kwamba Yohana amefufuka katika wafu, 8 na wengine ya kwamba Eliya ametokea, na wengine ya kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. 9 Lakini Herode akasema, Yohana nilimkata kichwa; basi ni nani huyu ambaye ninasikia mambo haya juu yake? Akataka kumwona. 10 Basi wale mitume waliporudi walimweleza mambo yote waliyoyatenda; akawachukua, akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida. 11 Na makutano walipojua walimfuata; akawakaribisha, akawa akisema nao habari za ufalme wa Mungu, akawaponya wale wenye haja ya kuponywa. 12 Na jua likaanza kushuka; wakamwendea wale Thenashara, wakamwambia, Uage mkutano, ili waende katika vijiji na mashamba ya kandokando wapate mahali pa kulala na vyakula, maana hapa tulipo ni nyika tupu. 13 Akawaambia, Wapeni ninyi chakula. Wakasema, Hatuna kitu zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, tusipokwenda tukawanunulie watu hawa wote vyakula. 14 Kwa kuwa wanaume waliokuwako walipata kama elfu tano. Akawaambia wanafunzi wake, Waketisheni watu kwa safu, kila safu watu hamsini. 15 Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote. 16 Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni akavibariki, akavimega, akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. 17 Wakala, wakashiba wote; na katika vile vipande vilivyowabakia walikusanya vikapu kumi na viwili. 18 Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwapo pamoja naye, akawauliza, Je! Makutano hao wanasema ya kuwa mimi ni nani? 19 Wakamjibu wakisema, Yohana Mbatizaji; lakini wengine, Eliya; na wengine kwamba mmojawapo wa manabii wa kale amefufuka. 20 Akawaambia, Nanyi mwasema ya kwamba mimi ni nani? Petro akamjibu akasema, Ndiwe Kristo wa Mungu. 21 Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; 22 akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. 23 Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. 24 Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. 25 Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe? 26 Kwa sababu kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. 27 Nami nawaambia kweli, Wapo katika hawa wanaosimama hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata wauone kwanza ufalme wa Mungu. 28 Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. 29 Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. 30 Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; 31 walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. 32 Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. 33 Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. 34 Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. 35 Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. 36 Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona. 37 Ikawa siku ya pili yake, waliposhuka mlimani, mkutano mkubwa ulikutana naye. 38 Na tazama, mtu mmoja katika mkutano alipaza sauti, akisema, Mwalimu, nakuomba umwangalie mwanangu; kwa kuwa yeye ni mwanangu pekee. 39 Na tazama, pepo humpagaa, naye mara hupiga kelele; tena humtia kifafa, huku anatokwa na povu, wala hamwachi ila kwa shida, akimchubua-chubua. 40 Nikawasihi wanafunzi wako wamtoe, wasiweze. 41 Yesu akajibu akasema, Enyi kizazi kisicho na imani, kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwachukulia hata lini? Mlete mwanao hapa. 42 Alipokuwa katika kumwendea, pepo akambwaga chini, akamtia kifafa. Yesu akamkemea pepo mchafu, akamponya mtoto, akamrudishia babaye. 43 Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu. Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake, 44 Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. 45 Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile. 46 Wakaanza kuhojiana, ni nani atakayekuwa mkubwa miongoni mwao. 47 Naye Yesu alipotambua mawazo ya mioyo yao, alitwaa mtoto mdogo akamweka karibu naye, 48 akawaambia, Ye yote atakayempokea mtoto huyu kwa jina langu anipokea mimi; na ye yote atakayenipokea mimi ampokea yeye aliyenituma. Kwa kuwa aliye mdogo miongoni mwenu nyote huyo ndiye mkubwa. 49 Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. 50 Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu. 51 Ikawa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, yeye aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; 52 akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. 53 Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. 54 Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]? 55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.] 56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine. 57 Nao walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata ko kote utakakokwenda. 58 Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. 59 Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusa kwanza niende nikamzike baba yangu. 60 Akamwambia Waache wafu wawazike wafu wao; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. 61 Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. 62 Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.

Cette Bible est dans le domaine public.