Un clic sur un verset envoie vers le comparateur de versions.
Matthieu 26.2 Bible en Swahili de l’est
Mort et résurrection de Jésus
Complot contre Jésus
Voir Matthieu 26.1 en vidéo
1 Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake, 2 Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulibiwe. 3 Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; 4 wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua. 5 Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.
Une femme verse du parfum sur Jésus
6 Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma, 7 mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani. 8 Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu? 9 Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini. 10 Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi. 11 Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote. 12 Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu. 13 Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake. 14 Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, 15 akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. 16 Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.
Institution de la cène
17 Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? 18 Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. 19 Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. 20 Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. 21 Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. 22 Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? 23 Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. 24 Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. 25 Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
Voir Matthieu 26.26 en vidéo
26 Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu 27 Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; 28 kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. 29 Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu. 30 Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. 31 Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. 32 Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. 33 Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. 34 Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. 35 Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.
Arrestation de Jésus
36 Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. 37 Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. 38 Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. 39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. 40 Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu. 42 Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. 43 Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito. 44 Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale. 45 Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi. 46 Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia.
Voir Matthieu 26.47 en vidéo
47 Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu. 48 Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni. 49 Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu. 50 Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu. 51 Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. 52 Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga. 53 Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika? 54 Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri? 55 Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate. 56 Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Jésus devant le conseil juif
57 Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee. 58 Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho. 59 Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; 60 wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. 61 Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. 62 Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? 63 Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu. 64 Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni. 65 Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake; 66 mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa. 67 Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi, 68 wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga? 69 Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya. 70 Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo. 71 Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti. 72 Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu. 73 Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha. 74 Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo. 75 Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.